Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, katika kuendeleza mikutano na vikao vya Mkuu wa Kamati ya Arubaini ya Hawza za nchini Iraq, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mousavizadeh alikutana na kufanya mazungumzo na kundi la masheikh pamoja na viongozi wa makabila wa Mkoa wa Al-Muthanna.
Mwanzoni mwa kikao hicho, masheikh na viongozi wa eneo hilo walitoa salamu za ukaribisho na kusisitiza juu ya undani wa uhusiano wa kiitikadi na wa kihistoria kati ya mataifa ya Iran na Iraq. Wakiashiria mshikamano wa mataifa hayo mawili katika nyakati mbalimbali muhimu, walisema: "Vita vyenu ni vita vyetu, hasara yenu ni hasara yetu, na sisi sote tupo katika handaki moja." Masheikh wa Mkoa wa Al-Muthanna walieleza kuwa mshikamano huo unatokana na imani ya pamoja, mapenzi kwa Ahlul-Bayt (as), na uzoefu wa miaka mingi wa kuandamana pamoja na kufanya jihadi. Aidha walisisitiza kwamba hakuna njama yoyote inayoweza kuwatenganisha watu wa mataifa haya mawili ya kindugu.
Katika muendelezo wa mkutano huo, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mousavizadeh, akitoa shukrani kwa ushiriki mkubwa wa wananchi wa Iraq katika hafla ya mazishi ya Kiongozi Shahidi, alieleza kuwa ushiriki huo ulikuwa ni kielelezo cha uaminifu, udugu wa Kiislamu na mshikamano wa kina kati ya mataifa hayo mawili. Alisema: Ushiriki huo wa kishindo ulipeleka ujumbe wa wazi kwa ulimwengu kuhusu umoja wa Umma wa Kiislamu na ukawa sababu ya hasira na kushindwa maadui ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakijaribu kuleta mgawanyiko kati ya mataifa ya Iran na Iraq.
Aliongeza: Mazishi hayo makubwa yaliyofanyika nchini Iraq, katika kipindi cha kuelekea Arubaini ya Imam Hussein (as), yalikuwa ni dhihirisho halisi la mshikamano na umoja wa Umma wa Kishia; taswira iliyoonesha kwamba Mashia, licha ya mipaka ya kijiografia, wana utambulisho mmoja, lengo moja na safu moja.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mousavizadeh pia, akirejelea ushiriki mkubwa wa wananchi wa Iran katika shughuli zinazohusiana na Kiongozi Shahidi, alisema: Ushiriki huo mkubwa haukuwa harakati ya kisiasa wala hatua ya kiserikali, bali ulikuwa ni dhihirisho la mapenzi, imani na mafungamano ya moyoni ya wananchi kwa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na maadili ya dini; ushiriki ambao ulionesha mtaji wa kijamii usio na mfano.
Mkurugenzi wa Idara ya Tablighi katika Masuala ya Kimataifa ya Hawza, akizungumzia misimamo ya uadui ya maadui hususan Marekani, alisema: Kinachowakasirisha na kuwatia hofu maadui si nguvu za kijeshi wala za kiuchumi, bali ni umoja na mshikamano wa mataifa ya Iran na Iraq. Wanafahamu vyema kwamba uhusiano huu wa kina umefanya mipango yao mingi ishindwe kutekelezwa.
Alisema kuwa mtaji mkubwa wa leo wa Umma wa Kiislamu ni umoja na mshikamano wa mataifa ya Iran na Iraq, na akaongeza: Mtaji huu wenye thamani ni matokeo ya miaka mingi ya kujitolea na mapambano, pamoja na baraka za harakati kubwa ya Arubaini ya Imam Hussein (as); harakati ambayo imezikaribisha nyoyo za watu na kuimarisha zaidi safu ya Muqawama.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mousavizadeh, akizungumzia shakhsia ya Kiongozi Shahidi, alielezea maisha yake ya unyenyekevu na zuhudi kuwa miongoni mwa sifa zake muhimu za kimaadili na kusema: Kiongozi Shahidi aliishi maisha yake kwa unyenyekevu wa hali ya juu na alifikia daraja ya ushahidi akiwa katika nyumba yake na makazi yake ya kizuhudi, si katika majumba ya kifahari wala maficho salama. Mtindo huo wa maisha ndio uliowafanya watu wa mataifa mbalimbali waamini uaminifu na ikhlasi yake, na ukawa chanzo cha msukumo kwao.
Mwishoni, Mkuu wa Kamati ya Arubaini ya Hawza, huku akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi umoja na mshikamano wa Umma wa Kishia, alisema: Leo, tunapaswa kushikamana na mafundisho ya Ahlul-Bayt (as) na kudumisha mshikamano kati ya mataifa ya Kiislamu ili kuimarisha safu moja ya Umma wa Kiislamu, kwa lengo la kusimama imara mbele ya maadui, kuandaa mazingira ya ushindi wa haki, na kujiandaa kwa ajili ya kudhihiri kwa Imam wa Zama, Hadhrat Waliyul-'Asr (aj).
Maoni yako